Nchi yetu (Tanzania) huzalisha nguvu kazi kubwa kila mwaka.
Vyuo vikuu, vyuo vya kati, sekondari na shule za msingi hutiririsha wahitimu
wengi sokoni zaidi ya hitaji la soko kwa mwaka husika hali ambayo hupelekea
wengi kukosa ajira rasmi kwakuwa supply ni kubwa kuliko demand. Ukosefu wa
ajira rasmi hupelekea wahitimu wa kada mbalimbali kukaa nyumbani na kusubiri
kuajiriwa. Wengi wao hutamani kujiajiri lakini changamoto au vikwazo
vitokanavyo na kujiajiri huwakatisha tama. Vikwazo hivyo ni kama:
- Ukosefu wa mtaji
- Elimu ya ujasiriamali
- Vikwazo vya kimfumo
- Hofu n.k
- Mara nyingi mtu aliyesoma anatamani kufanya mambo makubwa ili jamii imuone kweli amesoma na anafanya mambo ya maana. Watu wengi wanaweza kumiliki simu ya laki moja au mbili lakini haoni kama hiyo hela inaweza kumsaidia kuanza biashara ndogo hatimae ikawa kubwa. Swali linalokuja kichwani mwa mtu ni kuwa watanionaje mimi msomi nauza mchicha?
- Hofu ya kushindwa, hii huwapata hata wale ambao wako kwenye ajira na wanatamani kuwekeza kile wanachopata kutoka kazini. Wengi huanza kuwaza mabaya badala ya kuwaza mema hali ambayo hupelekea kushindwa kuanzisha biashara
- Hofu ya kimashindano, tatizo la watu wengi tunapenda kujilinganisha na watu wengine (kushindana). Kujiajiri kunataka kujitoa, kujinyima na uvumilivu wa muda mrefu ili kufikia malengo si kama kuajiriwa. Wengi hutamani mafanikio ya haraka haraka ili aonekane kuwa ni mtu aliyefanikiwa mbele ya marafiki zake au wale aliosoma nao kwahiyo wengi huona ni vigumu kujiajiri kwa kuwa hakuwezi kumpa pesa za chapchap
- Hofu ya kutokuamini vipawa walivyo navyo. Siku moja Mwl. Christopher Mwakasege alihubiri akisema, inawezekanaje Mungu kuweka wazo moja la kuajiriwa ndani ya wahitimu wote? Akasema haiwezekani ina maana kuna wengine wamebeba mawazo ambayo si ya kwao (au ambayo si mpango wa Mungu). Sio lazima wote kuajiriwa na wala si mpango wa Mungu wote kuajiriwa, ndio maana Mungu aliweka vipawa mbalimbali ndani yetu ili vitusaidie kujiajiri.
Hitimisho, ni lazima kumshinda adui hofu ili uweze kuvuka
kiunzi cha kukosa ajira katika sekta rasmi la sivyo miaka itaenda utajikuta mtu
wa kushinda nyumbani ukingoja kuajiriwa. Tafuta kitu chochote cha kufanya hata
kama watu watakudharau na kukucheka usiogope maadamu unajua ufanyacho.

No comments:
Post a Comment