Siku ya leo tunaangazia aina ya biashara ndogondogo ambazo mtu anazoweza
kuzifanya na zikamuingizia kipato. Kabla ya kuziangalia ni vyema nikumbushe
kuwa hata mbuyu ulianza kama mchicha, pia matajiri wote tunaowaona leo hii
asilimia kubwa walianzia katika biashara ndogo ndogo hatimae zikakuwa na kuwa
kubwa ambazo siku za leo tunapeleka CV zetu ili watuajiri. Hivyo kitu kikubwa
ni kujua nini unafanya na kujiwekea malengo ambayo unatamani kuyafikia. Zipo
biashara ndogo ndogo ambazo nimezifanyia utafiti katika mkoa ninaoishi na ukizifanya kwa kumaanisha zinaweza kukuinua na
kukufikisha mbali/mahali unapotamani kwenda, nazo ni hizi zifuatazo
- Kutengeneza mandazi na kusambaza madukani
- Kuuza nafaka (rejareja)
- Kuuza maziwa
- Kuuza matunda na mbogamboga
- Kuuza pumba
Kutengeneza mandazi,
vitumbua na kusambaza madukani
Kipindi mimi nakua miaka ya nyuma biashara hii ilikuwa
inafanywa na kina mama lakini siku za leo inafanywa na bakery ambazo zimejaa mitaani.
Hii ni biashara ambayo haihitaji mtaji mkubwa na ina mzunguko mzuri kama
utafanikiwa kupata masoko pia ukiwa na utaalamu unaotakiwa pamoja na bidhaa
nzuri. Vifaa inavyohitaji ni kama kalai, meza, sanduku la mbao la kukandia ngano, trei na sanduku la mbao la kuhifadhia mandazi.
Kwa ujumla vifaa vinavyotakiwa havizidi laki 2 tukiacha
malighafi. Unaweza kuajiri kijana wa kusambaza au ukafanya wewe mwenyewe.
Katika mfuko mmoja wa ngano unaweza kupata 15,000 hadi 20,000 kama faida.
(Maelezo haya nimepewa na Bw. Shedrack ambaye anajishughulisha na biashara hii
katika mji wa Bukoba)

