Thursday, September 10, 2015

Fahamu Aina ya Biashara Ndogo Ndogo Zinazoweza Kukuingizia Kipato

Siku ya leo tunaangazia aina ya biashara ndogondogo ambazo mtu anazoweza kuzifanya na zikamuingizia kipato. Kabla ya kuziangalia ni vyema nikumbushe kuwa hata mbuyu ulianza kama mchicha, pia matajiri wote tunaowaona leo hii asilimia kubwa walianzia katika biashara ndogo ndogo hatimae zikakuwa na kuwa kubwa ambazo siku za leo tunapeleka CV zetu ili watuajiri. Hivyo kitu kikubwa ni kujua nini unafanya na kujiwekea malengo ambayo unatamani kuyafikia. Zipo biashara ndogo ndogo ambazo nimezifanyia utafiti katika mkoa ninaoishi na  ukizifanya kwa kumaanisha zinaweza kukuinua na kukufikisha mbali/mahali unapotamani kwenda, nazo ni hizi zifuatazo
  • Kutengeneza mandazi na kusambaza madukani
  • Kuuza nafaka (rejareja)
  • Kuuza maziwa
  • Kuuza matunda na mbogamboga
  • Kuuza pumba

Kutengeneza mandazi, vitumbua na kusambaza madukani

Kipindi mimi nakua miaka ya nyuma biashara hii ilikuwa inafanywa na kina mama lakini siku za leo inafanywa na bakery ambazo zimejaa mitaani. Hii ni biashara ambayo haihitaji mtaji mkubwa na ina mzunguko mzuri kama utafanikiwa kupata masoko pia ukiwa na utaalamu unaotakiwa pamoja na bidhaa nzuri. Vifaa inavyohitaji ni kama kalai, meza, sanduku la mbao la kukandia ngano, trei na sanduku la mbao la kuhifadhia mandazi.

Kwa ujumla vifaa vinavyotakiwa havizidi laki 2 tukiacha malighafi. Unaweza kuajiri kijana wa kusambaza au ukafanya wewe mwenyewe. Katika mfuko mmoja wa ngano unaweza kupata 15,000 hadi 20,000 kama faida. (Maelezo haya nimepewa na Bw. Shedrack ambaye anajishughulisha na biashara hii katika mji wa Bukoba)

Kikwazo kikubwa Kinachofanya Watu Wengi Wategemee Kuajiriwa

Nchi yetu (Tanzania) huzalisha nguvu kazi kubwa kila mwaka. Vyuo vikuu, vyuo vya kati, sekondari na shule za msingi hutiririsha wahitimu wengi sokoni zaidi ya hitaji la soko kwa mwaka husika hali ambayo hupelekea wengi kukosa ajira rasmi kwakuwa supply ni kubwa kuliko demand. Ukosefu wa ajira rasmi hupelekea wahitimu wa kada mbalimbali kukaa nyumbani na kusubiri kuajiriwa. Wengi wao hutamani kujiajiri lakini changamoto au vikwazo vitokanavyo na kujiajiri huwakatisha tama. Vikwazo hivyo ni kama:     
  • Ukosefu wa mtaji  
  • Elimu ya ujasiriamali  
  • Vikwazo vya kimfumo 
  • Hofu n.k